Exodus 4

Ishara Za Musa

1 aMusa akamjibu, “Itakuwaje kama hawataniamini au kunisikiliza, waseme, ‘Bwana hakukutokea’?”

2 bNdipo Bwana akamwambia, “Ni nini hicho kilicho mkononi mwako?”

Akajibu, “Fimbo.”

3 c Bwana akasema, “Itupe chini.”

Musa akaitupa chini hiyo fimbo nayo ikawa nyoka, naye akaikimbia.
4Kisha Bwana akamwambia, “Nyoosha mkono wako umkamate mkiani.” Basi Musa akanyoosha mkono akamkamata yule nyoka, naye akabadilika tena kuwa fimbo mkononi mwake. 5 d Bwana akasema, “Hivi ndivyo Waisraeli watakavyoamini kuwa Bwana, Mungu wa baba zao, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo, amekutokea wewe.”

6 eKisha Bwana akamwambia, “Weka mkono wako ndani ya joho lako.” Basi Musa akaweka mkono wake ndani ya joho lake, naye alipoutoa, ulikuwa na ukoma, mweupe kama theluji.

7 fMungu akamwambia, “Sasa urudishe tena huo mkono ndani ya joho lako.” Basi Musa akaurudisha mkono wake ndani ya joho lake na alipoutoa, ulikuwa mzima, kama sehemu zingine za mwili wake.

8 gNdipo Bwana akamwambia, “Kama hawatakuamini wewe, au kutojali ishara ya kwanza, wataamini ishara ya pili. 9 hLakini kama hawataamini ishara hizi mbili au hawatawasikiliza ninyi, chukua kiasi cha maji kutoka Mto Naili uyamimine juu ya ardhi kavu. Maji mtakayotoa mtoni yatakuwa damu juu ya ardhi.”

10 iMusa akamwambia Bwana, “Ee Bwana, kamwe sijapata kuwa msemaji kwa ufasaha wakati uliopita wala tangu ulipoanza kuzungumza na mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito kuzungumza.”

11 j Bwana akamwambia, “Ni nani aliyempa mwanadamu kinywa? Ni nani aliyemfanya mtu kuwa kiziwi au bubu? Ni nani anayempa mtu kuona au upofu? Je, si mimi, Bwana? 12 kSasa nenda, nitakusaidia kusema, nami nitakufundisha jambo la kusema.”

13 lLakini Musa akasema, “Ee Bwana, tafadhali mtume mtu mwingine kufanya kazi hiyo.”

14 mNdipo hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Musa, akamwambia, “Vipi kuhusu ndugu yako, Haruni Mlawi? Ninajua yeye anaweza kuzungumza vizuri. Naye yuko tayari njiani kukulaki, na moyo wake utafurahi wakati atakapokuona. 15 nUtazungumza naye na kuweka maneno kinywani mwake. Nitawasaidia ninyi wawili kusema, nami nitawafundisha jambo la kufanya. 16 oHaruni ataongea na watu badala yako na itakuwa kwamba yeye amekuwa kinywa chako nawe utakuwa kama Mungu kwake. 17 pLakini chukua fimbo hii mkononi mwako ili uweze kuitumia kufanya ishara hizo za ajabu.”

Musa Anarudi Misri

18Kisha Musa akarudi kwa Yethro mkwewe akamwambia, “Niruhusu nirudi kwa watu wangu Misri kuona kama yuko hata mmoja wao ambaye bado anaishi.”

Yethro akamwambia, “Nenda, nami nakutakia mema.”

19 qBasi Bwana alikuwa amemwambia Musa huko Midiani, “Rudi Misri kwa maana watu wote waliotaka kukuua wamekufa.” 20 rBasi Musa akamchukua mkewe na wanawe, akawapandisha juu ya punda na kuanza safari kurudi Misri. Naye akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake.

21 s Bwana akamwambia Musa, “Utakaporudi Misri, hakikisha kwamba utafanya mbele ya Farao maajabu yote niliyokupa uwezo wa kuyafanya. Lakini nitafanya moyo wake kuwa mgumu ili kwamba asiwaruhusu watu waende. 22 tKisha mwambie Farao, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Israeli ni mwanangu mzaliwa wa kwanza, 23 unami nilikuambia, “Ruhusu mwanangu aondoke, ili aweze kuniabudu mimi.” Lakini ukakataa kumruhusu kwenda, basi nitaua mwana wako mzaliwa wa kwanza.’ ”

24 vMusa alipokuwa mahali pa kulala wageni akiwa njiani kurudi Misri, Bwana akakutana naye, akataka kumuua. 25 wLakini Sipora akachukua jiwe gumu, akakata govi la mwanawe na kugusa nalo miguu ya Musa. Sipora akasema, “Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu.” 26Sipora alipomwita Musa, “Bwana arusi wa damu,” alikuwa anamaanisha ile tohara. Baada ya hayo Bwana akamwacha.

27 x Bwana akamwambia Haruni, “Nenda jangwani ukamlaki Musa.” Basi akakutana na Musa kwenye mlima wa Mungu, akambusu. 28Kisha Musa akamwambia Haruni kila kitu Bwana alichomtuma kusema, vilevile habari za ishara na maajabu alizokuwa amemwamuru kufanya.

29 yMusa na Haruni wakawakusanya wazee wote wa Waisraeli, 30naye Haruni akawaambia kila kitu Bwana alichokuwa amemwambia Musa. Pia akafanya ishara mbele ya watu, 31 znao wakaamini. Nao waliposikia kuwa Bwana anajishughulisha nao, na kwamba ameona mateso yao, walisujudu na kuabudu.
Copyright information for SwhKC